Mada: vifo vya gafla kwa kuku
Nimatumaini yangu ndugu msomaji, u mzima wa afya njema kwa kadri Mungu alivyokujalia kuamka salama. Ni muhimu kwangu kuhakikisha unapata taaeifa sahihi kuhusiana na ufugaji wa kuku aina zote. Leo nimependa kukuletea somo muhimu sana kwako kama linavyojieleza hapo juu.
Niingie moja kwa moja kwenye somo la leo, kuku ni ndege mchangamfu sana katika ubora wa afya yake. Mara nyingi kuku akiwa anaumwa kuna dalili mbalimbali atazionyesha ili kama mfugaji ukiwa makini ni rahisi kutambua na kumsaidia au kumtibu.
Zifuatazo ni dalili mbalimbali ambazo utaziona kwa kuku wako ili ujue ni ugonjwa gani.
1.Kuku kuzubaa ni moja ya dalili isiyo ya kawaida kwa kuku. Mara zote kuku ni mchangamfu sana kufikia kwamba hawezi tulia sehemu moja. Kwa hiyo ukiona kuku wako amezubaa kwa muda mrefu ujue kuna tatizo, hivyo ni muhimu kuchunguza tatizo ni nini ili uweze kumtibu kwa wakati kabla madhara makubwa kutokea. Mfano, siku moja nilikuta kuku wangu kazubaa. Ikabidi nimfuatie kwa muda lakini sikufanikiwa kugundua chochote au tatizo, maana sikuwa nae muda mwingi. Ikabidi nifanye maamuzi ya kumchinja, nilichokikuta ndani ya tumbo la kuku huyo ni utumbo pamoja na firigisi vimeoza japokuwa kuku alikuwa hai kabla ya kuchinjwa.
2.Kujitenga kwa kuku ni tabia ya tofauti kabisa kwa kuku. Kuku hupenda kukaa pamoja na wenzie muda mwingi wakicheza na kula chakula pamoja na wenzie ndio sifa yake. Kujitenga maana hanafuraha yoyote ya kushiriki na wenzie. Kimsingi hapo utakuta anasumbuliwa na mafua na kukaa pembeni. Muda mwingine unaweza mshika na asishituke kabisa. Hapo mfugaji chukua hatua.
3. Kushusha mabawa ni dalili nyingine ambayo kuku huonyesha pale ambapo hayuko sawa kiafya. Kuku mwenye afya njema mabawa pamoja na mkia wake vinakuwa juu na kucheza cheza kuashiria kuwa anafuraha na afya njema kabisa. Mtazame kuku wako takribani dakika 15 hadi 30 kwa siku ilikufuatilia kama wako salama.
4. Rangi ya kinyesi cha kuku ni mojawapo ya dalili muhimu sana katika ufugaji bora wa kuku wako. Kuku mwenye afya njema hijisaidia kinyesi cha rangi nyeusi na mara nyingine. Imechanganyika na kijani kidogo. Hivyo tofauti na rangi hizo, rangi nyingine huashiria magonjwa mbalimbali. Mfano, kuna kinyesi cha rangi ya njano, nyeupe, brown, kijivu na kijani tupu.
5. Kukosa hamu ya kula ni mojawapo ya dalili muhimu kujua na kwa leo itakuwa dalili ya mwisho katika zilizoorodheshwa lakini sio ya mwisho kabisa zipo nyingine nyingi sana. Kuku kwa tabia yao hupenda kula muda wote ni mara chache sana kukuta ametulia au kupumzika kula.hivyo ukiona umekaa dakika 15 hadi 30, kuku hali chochote hapo kuna tatizo ni vyema ukachukua hatua.
Tunawajibika kufanya yafuatayo kwa ajili ya kuboresha ufugaji wetu.
Kuwafuatilia kuku wako kwa karibu. Holi jambo ni muhimu sana kwa mfugaji na pia ni wajibu kama unatarajia zao bora. Jiwekee muda fulani kwa siku takribani saa nzima kukaa ukiwaangalia kuku wako na kuona kama wanaendeleaje? Kuna tabia ya wafugaji wengi kuwa achia vijana wao wa kazi au vibarua kufuatilia mifugo yake na yeye kusimamia kwa simu na kubaki kuwa mtu wa kupewa ripoti. Hili jambo haliwezi kuleta mazao chanya na bora, pata muda wa kufuatilia kwa karibu ili kama kuna tatizo utagundua tu kirahisi na kulifanyia kazi.
Lingine ni kuwa wa kwanza kufika bandani asubuhi kabla ya kuwafungulia kuku wako nje. Jambo hili ni muhimu sana kwa mfugaji. Maana utagundua mambo mengi yatakayo kusaidia katika ufugaji wako. Mfano, ni muhimu kuangalia kinyesi cha kuku walichojisaidia usiku kuamkia siku hiyo. Pia kutazama kuku wako wamechangamka n.k
Napenda kukushukuru ndugu msomaji wa makala hii kwa kuwa nami tangu mwanzo wa makala hii hadi kufikia hapa. Nimatumai yangu utakuwa umejifunza kitu. Karibu sana kuendelea kujifunza katika makala zijazo siku kama hii wiki ijayo. Asanteni
Comments
Post a Comment