Mkojo wa sungura sasa watibu mazao Njombe
Mkojo wa sungura sasa watibu mazao Njombe
Mtanzania17 Jan 2018Na ELIZABETH KILINDI
UMOJA wa wajasiriamali wanaojishughulisha na kilimo biashara Mkoa wa Njombe (Vibinjo), wameachana na matumizi ya dawa za madukani zenye kemikali za kuulia wadudu, kukuzia mazao pamoja na mbolea, badala yake wanatumia mkojo wa sungura kutibu magonjwa hayo.
Wakizungumza na MTANZANIA jana, wanachama hao walisema wamepata elimu kutoka kwa viongozi wao na hivyo wamefanya majaribio na kubaini ukweli kwamba mkojo wa sungura unaweza kutumika kama mbolea, kukuzia pamoja na dawa ya kuulia wadudu.
Obeid Changula alisema baada ya kupata elimu ya matumizi ya mkojo huo, ilimlazimu kufanya majaribio katika mazao yake, ikiwemo mahindi na kubaini ukweli huo na hivyo hawatumii dawa zenye kemikali kuendeshea kilimo chao.
“Nilivyopata hii elimu nilirudi shambani kwangu ambako mahindi yangu yalikuwa yameanza kushambuliwa yakiwa bado machanga, yalikuwa yamedhoofu kwani wadudu walikuwa wameanza kula chini ya mizizi.
“Hivyo nikachukua mkojo wa sungura lita moja nikachanganya na maji ndoo ya lita 10, unachanganya baada ya hapo unanyunyuzia, mazao yangu yalibadilika kabisa,” alisema Changula.
Aliongeza baada ya kunyunyuzia katika mahindi yake, yalibadilika na kuwa yenye ubora na kubaini pia kuwa mkojo huo ni mbolea licha ya kuua wadudu na pia unakuza mazao.
Lusia Mgaya ambaye pia ni mwanakikundi, alisema mkojo wa sungura unatumika katika mazao mbalimbali na unatumia kupulizia mara moja kwa mwaka kwa yale mazao ya muda mrefu.
“Mkojo wa sungura umekuwa faida kwetu hivi sasa, hatutumii dawa zenye kemikali kwenye mazao yetu badala yake mkojo huu unatusaidia, tunashukuru aliyetupa hii elimu na tumeona kwa kujaribu sisi wenyewe,” alisema Lusia.
Mjumbe wa Bodi wa Umoja huo, Lucius Chambiaga, alisema mkojo wa sungura una viuatilifu vingi ambavyo vinasababisha kuwa mbolea, kukuzia pamoja na dawa ya kuulia wadudu.
Alisema awali walibaini uwepo wa soko la uhakika la sungura lipo nchini Kenya, lakini wamekuja kubaini jambo hilo ambalo ni jema sana kwao.
Comments
Post a Comment