FAIDA YA KUKU
FAIDA ZA UFUGAJI KUKU WA ASILI
1. Chakula – nyama ya kuku na mayai hutumika kama chakula muhimu cha wanadamu, chenye protini.
2. Chanzo cha kipato – mkulima hupata fedha akiuza kuku au mayai.
3. Chanzo cha ajira – ufugaji wa kuku hutoa ajira kwa jamii.
4. Kuku hutumika kwenye shughuli za ndoa kama vile kutoa mahari na pia ni kitoweo muhimu katika sherehe hizo.
5. Gharama nafuu za kuanzisha na kuendesha mradi huu.
6. Ni kitoweo rahisi na chepesi kwa wageni kuliko wanyama wakubwa kama ng’ombe au mbuzi.
7. Ni kitoweo kisichohitaji hifadhi, hutumika mlo mmoja au miwili na kumalizika.
8. Kuku na mayai hutumika kwa tiba za asili.
9. Jogoo hutumika kama saa anapowika nyakati za alfajiri na majira mengine ya siku. Hutuhabarisha iwapo kiumbe kigeni au cha hatari kwa mlio maalum wa kuashiria hatari.
11. Soko lipo la uhakika, ukilinganisha na kuku wa kisasa kwani nyama na mayai yake hupendwa zaidi na walaji.
12. Manyoya ya kuku hutumika kama mapambo, pia huweza kutumiaka kutengenezea mito ya kulalia na kukalia.
13. Shughuli za utafiti – kuku wanatumika katika tafiti nyingi za baiolojia, kama kutambua mambo ya lishe.
14. Shughuli za viwandani:
Mayai yenye mbegu ya jogoo hutumika katika kutengeneza dawa za chanjo.
Magamba ya mayai yanaweza kutumika katika utengenezaji wa vyakula vya wanyama.
Kiini cha njano cha mayai kinaweza kutumika kutengeneza mafuta ya kuoshea nywele (shampoo).
MAPUNGUFU YA KUKU WA ASILI
1. Hutaga mayai madogo wastani wa gramu 47 ambapo kuku wa kisasa wastani wa gramu 55, aidha hutaga mayai machache wastani wa mayai 60 kwa mwaka ambapo kuku wa kisasa huweza kutaga hadi mayai 300 kwa mwaka.
2. Ukuaji taratibu – kuku wa asili hukua taratibu kutokana na lishe duni. Kutokana na hali hiyo kuku huchukua muda mrefu (miezi sita) kufikia uzito wa kuchinjwa (kilo 1 - 1.5). Hali hii pia hufanya faida ya ufugaji wa kuku wa asili kuchukua muda mrefu
kupatikana.
3. Nyama yake ni ngumu (huchukua muda mrefu kuiva) ikilinganishwa na kuku wa kisasa.
CHANGAMOTO KATIKA UFUGAJI KUKU WA ASILI
1. Mabanda: Ukosefu wa mabanda bora.
2. Wezi, wanyama na ndege hushambulia kuku.
3. Magonjwa: kama mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku.
4. Tabia na miiko ya baadhi ya jamii. Baadhi ya jamii za makabila hapa nchini huona ufugaji wa kuku kama ni kitu duni.
5. Upatikanaji haba wa chanjo za magonjwa kama vile, mdondo, ndui, homa ya matumbo.
KATIKA KUWAENDELEZA KUKU WA KIENYEJI NI VYEMA
1. Wajengewe nyumba bora
2. Wapewe kinga dhidi ya ugonjwa wa Mdondo (New Castle), GUMBORO , Ndui (Fowl Pox) pamoja na kinga ya minyoo.
3. Malezi bora ya vifaranga
4. Kuwapatia chakula cha ziada pamoja na maji ya kunywa ya kutosha.
Comments
Post a Comment