MENGINEYO: JINSI YA KUTENGENEZA MBOLEA YA MAJI
Mimea inaweza kukuonyesha inahitaji
nini. Ni rahisi sana kugundua endapo mimea haipati virutubisho vya
kutosha. Majani kubadili rangi ni ishara tosha kuwa mimea ina upungufu
wa virutubisho. Ni lazima mkulima awe tayari kutatua tatizo hilo kwa
haraka kabla hali haijawa mbaya. Upungufu wa madini ya nitrojen na
fosiforasi ni jambo la kawaida kwa mimea. Virutubisho hivi vinahitajik
kwa kiasi kikubwa sana kwenye mimea hasa katika hatua ya ukuaji.
Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kwamba
utatuzi unategemea hatua za kutunza udongo kwa kipindi chote cha mwaka.
Lisha udongo ili ulishe mazao yako; tumia mboji, samadi, mbolea vunde,
matandazo na utaratibu mzuri wa kupanda mazao kwa mzunguko.
Kunyunyizia kunafaa zaidi
Mkulima anaweza kusaidia hatua hii ya
kulisha mimea inayokuwa kwa njia ya kunyunyizia mbolea ya maji.
Kunyunyizia inasaidia kuipatia mimea virutubisho moja kwa moja kupitia
kwenye majani na shina.
Unaweza kuona matokeo mazuri ya kuweka
mbolea kwa kunyunyizia kulingana na kiwango cha mavuno, uwezo wa mimea
kukabiliana na wadudu pamoja na magonjwa, kuvumilia ukame, na kuongeza
ubora wa mazao. Mimea inakuwa na uwezo wa kunyonya mbolea mara 20 zaidi
ya unapotumia aina nyinginezo za uwekaji wa mbolea kwenye mimea.
Kutengeneza mbolea ya maji
Aina hii ya mbolea hutengenezwa kwa
kuchukua kiroba kilichojazwa samadi, aina mbalimbali ya mimea yenye
virutubisho na inayoaminika kuwa dawa ya mimea. Kiroba hicho kinafungwa
kwenye kijiti, na kutumbukiza kwa kuning’inia kwenye pipa lililojazwa
maji. Kiroba hicho ni lazima kichukue kati ya kilo 30-50 za samadi
pamoja na aina nyingine za mimea kwa maji lita 200 (tazama mchoro).
Mkulima anaweza kushika upande mmoja wa
mti na kunyanyua na kushusha kila baada ya siku tano ili kuchanganya na
kuharakisha kutolewa kwa virutubisho zaidi. Kwa kawaida mchanganyiko huo
unakuwa na harufu kali sana maana Nitrojeni nyingi inayopatikana
hugeuka kuwa Amonia. Ni vizuri kufunika pipa ili kuzuia kuyeyuka kwa
nitrojeni. Harufu ikishaisha, ujue mbolea yako ipo tayari kwa matumizi.
Ongeza maji na utingishe vizuri kabla ya kutumia. Nyunyizia mimea yako
kila wiki mpaka utakapoona mabadiliko.
Tumia mimea peke yake
Kama unatengeneza mbolea ya maji kwa
kutumia mimea peke yake, inashauriwa kutumia aina nyingi za mimea kama
vile mivule, mibangi mwitu, majani ya minyanya, mwarobaini, mashona
nguo, pamoja na vitunguu saumu. Aina hii ya mimea inasaidia sana katika
kuzuia magonjwa, wadudu na kutoa virutubisho muhimu kwa mimea
vinavyosaidia mkulima kupata mazao bora bila gharama ya ziada ya kununua
virutubisho.
Vigezo vya kunyunyizia
Ili mbolea ya kunyunyizia iwe na matokeo mazuri, vigezo vifuatavyo vifuatwe:
• Inashauriwa kutumia mbolea iliyochanganywa vizuri ili kuepukana na kuunguza mimea.
• Acha maji utakayotumia kuchanganyia
mbolea yako nje katika pipa lililowazi usiku kucha, hii inasaidia kutoa
madini hatarishi, na kufanya mchanganyiko wenye faida kwa mimea.
• Tingisha vizuri. Chembechembe ndogo ambazo hazikuyeyuka zinaweza kuziba mdomo wa bomba la kunyunyizia.
• Matokeo mazuri yanaweza kupatikana endapo mbolea imechanganywa vizuri na kunyunyiziwa wakati hakuna upepo.
• Nyunyiza mbolea wakati wa asubuhi au jioni wakati hakuna joto na upepo ukiwa umepungua.
Jinsi ya kugundua upungufu wa virutubisho
Nitrogen
Dalili:
Mahindi, maharage na mboga hukua kwa taabu sana, majani yanakuwa na
kijani mpauko. Sukumawiki na kabichi majani yanakuwa na mchanganyiko
wa rangi ya njano. Majani ya chini ndiyo huathiriwa kwanza, na
kiwango cha maua kuchanua hupungua au kuchelewa.
Kutibu: Ongeza kiasi
cha kutosha cha mbolea za asili. Panda mimea inayosaidia kuongeza
nitrojen kama lablab, desmodium(figiri) na lusina. Weka mboji,
samadi na mbolea ya maji yenye nitrojen kwa wingi.
Phosphorous
Dalili: Mahindi,
maharage na mbogamboga haikui vizuri. Majani hugeuka na kuwa rangi
ya kijani kama bluu na zambarau. Matunda hubakia kuwa madogo. Inaweza
kuharibu mizizi au kukosekana kwa Nitrojeni.
Kutibu: Tumia mbolea ya Minjingu ambayo ina Phosphate, au tumia mbolea asili ya maji yenye phosphorus.
Potassium
Dalili: Majani
yanakuwa na rangi ya njano kama yanakauka kuzunguka. Kuchanua kwa
shida na kutokuwa mpango mzuri wa matunda. Mmea unashambuliwa na
magonjwa kirahisi.
Kutibu: Boresha udongo wako kwa kutumia mimea yenye virutubisho vya potassium au weke majivu kwenye shamba lako.
Comments
Post a Comment