KILIMO CHA MATANGO:-Fahamu Kilimo Cha Matango (Cucumber)
Fahamu Kilimo Cha Matango
(Cucumber)
Matango huwa tayari kuvunwa kuanzia siku 50 hadi 60, yaani mwezi
mmoja na nusu hadi miwili baada ya kupanda, na pia matunda yanatakiwa kuwa na
urefu wa sentimita 15 mpaka 20, urefu pia unaweza kutofautiana kulingana na
aina ya matango yaliyopandwa.
UTANGULIZI
Asili ya kilimo cha matango
inaaminika kuwa ni kaskazini magharibi mwa India ambako yamekuwa yakilimwa kwa
zaidi ya miaka thelathini sasa. Hata hivyo kwa sasa, matango, hustawishwa
katika sehemu nyingi za kitropiki. Matunda yake hukatwa katwa na kuliwa kama
achali, au kachumbari, au huwekwa kwenye siki na pia hupikwa na kuliwa.
Katika nchi yetu ya Tanzania matango
hulimwa katika mikoa ifuatayo: Tanga, Morogoro, Mbeya, Lindi, Mtwara na Pwani
ambako kuna jua la kutosha. Pia mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kilimo cha
matango hukubali.
Aina Za
Matango
Zipo aina nyingi za matango lakini
hutofautiana kwa umbo na rangi. Aina zinazojulika na kulimwa zaidi hapa kwetu
ni: Colorad, Telegraph, Palmetto, Chicago, Pickling, Straight 8 na Marketer.
Matumizi
Matango hutumiwa kama matunda na pia
ni aina ya mboga ambayo huongeza vitamin A, C na maji mwilini. Matunda haya
yanaweza kutumika pia kama saladi wakati wa mlo.
KUCHAGUA
ENEO NA KUANDAA SHAMBA
Eeo linatakiwa liwe na maji ya
kutosha na udongo wenye chachu (pH) ya 6.0 hadi 7.5 na hali ya joto wastani wa
nyuzi 20 hadi 25 zinahitajika kwa ukuaji bora. Matango hukua na kukomaa
kwa haraka zaidi katika udongo mwepesi, lakini hutoa mavuno makubwa zaidi
katika ardhi nzito kiasi. Hata hivyo ardhi inayotuamisha maji haifai kwa kilimo
cha matango, na ikibidi mimea ipandwe kwenye matuta.
Kabla ya kupanda udongo unatakiwa
utifuliwe vizuri na majani yaondolewe kabisa, usafi bustanini unashauriwa ili
kuondoa mimea mingine ambayo inaweza kuwa chanzo cha magonjwa.
Upandaji
Ni vizuri kama mkulima wa matango
akapanda mbegu moja kwa moja shambani, sia mbegu moja kiasi cha sentimita moja
chini ya udongo, na umbali kati ya mbegu na mbegu usipungue sentimita 30 na
zaidi.
Sehemu ya kupandia iwe na jua la
kutosha kwani matango huhitaji kiasi cha jua kisichopungua masaa 6 - 8 kwa
siku, mwagilia maji ya kutosha angalau mara moja kwa siku hasa nyakati za jioni.
Hii itasaidia ukuaji bora wa mazao yako hivyo kukuhakikishia mavuno mazuri.
Nafasi ya kupandia: sm 60 kati ya
mimea na sm 90 kati ya mistari.
Mbolea: Kabla ya kupanda weka
viganja 2 vya mbolea ya zizi katika kila shimo na changanya na udongo. Pia weka
kg 100 za NPK kwa hekta moja. Wiki tatu hadi nne baada ya kupanda: Weka mbolea
ya CAN kwa kiwango cha kijiko kimoja cha mezani kwa kila mmea (= gramu 10 kwa
mmea). Mbolea ni muhmu sana katika kilimo cha matango kwani zao hili pia
hutumia chakula kingi kutoka ardhini, hivyo muhimu kuweka samadi au mboji mara
kwa mara ili kuongeza chakula cha mmea.
Palizi
Palilia kila wakati magugu
yanapojitokeza, ni muhimu sana, hii husaidia kuepuka magonjwa na kushindania
chakula kati ya zao na magugu. Palizi hutakiwa kufanywa kwa kutumia jembe la
mkono ili kuepuka kuharibu mizizi.
Matandazo
(Mulching)
Baada ya kupalilia na kuweka mbolea
weka matandazo (mulch). Mkulima anaweza tumia nyasi au mabaki ya mimea mingine
kufunika ardhi, baada ya miche kutambaa kwa kiasi unaweza weka matandazo
kwaajili ya kuzuia upotevu wa unyevu, kupunguza uotaji wa magugu na pia
matandazo yakioza huongeza rutuba kwenye udongo na hulinda udongo dhidi ya
mmomonyoko.
Kita miti
(staking) ya kupandia: Chomeka miti ya kupandia matango yanayotambaa.
Hii husaidia matango yanayotambaa kupanda kufuata miti uliyoikita/chomeka.
MAGONJWA
Ni magonjwa machache tu yanayoathiri
kilimo cha matango, nayo ni:
(a) Mnyauko bacteria (Bacteria Wilt)
- hushambulia majani, majani yaliyoshambuliwa hudhoofu na hatimaye hufa. Mmea
ukikatwa huchuruzika ute mzito.
Kudhibiti
ugonjwa
Nyunyizia dawa ya Copper kila baada
ya siku 10 na tumia aina ya mbegu zenye uvumilivu mkubwa kama vile Palmetto.
(b) Ubwiri unga au ukungu (Powdery
Mildew) - Ukungu wake hushambulia majani na mashina.
Kudhibiti
Fanya usafi unaohitajika bustanini
mfano kuchoma taka. Pulizia Bayfidan.
(c) Magonjwa ya virusi (Cucumber
Mosaic Virus) – ugonjwa huu husababishwa na virusi, ikiwa mmea hautatibiwa
mapema, mmea hugeuka na kuwa wa njano, hudumaa na hushindwa kutoa matunda.
Ugonjwa huu pia huenezwa na magugu au wadudu kama vidukari na inzi weupe.
Kudhibiti
Weka shamba katika hali ya usafi, na
upande mbegu zinazovumilia ugonjwa. Nyunyizia dawa ya unga ya sulphur kila
baada ya siku 10.
WADUDU
(a) Dudu kobe wa matango - Huyu ni mdudu mbaya sana kwa matango kwani
hutafuna miche ya matango mara ichipuapo, pia hushambulia majani ya mimea
michanga na kuathiri ukuaji.
(b) Vidukari au wadudu mafuta (Aphids) - wadudu hawa hufyonza utomvu
kwenye majani machanga na kudumaza mmea kuufanya ushindwe kuzaa matunda.
Kudhibiti
Inabidi kutumia Malathion, Nicotine.
Hakisha dawa inafikia upande wa chini wa majani ili kuhakikisha wadudu wote
wamekufa.
(c) Buu au funza (Pickle Worm)
- Buu au funza hujipenyeza ndani ya ua, kisha huhamia kwenye tunda.
Kudhibiti
Tumia Rotenone au Crylite kila baada
ya juma moja.
Wadudu wengine ni kama minyoo ya
mizizi, na inzi weupe
KUVUNA
Matango huwa tayari kuvunwa kuanzia
siku 50 hadi 60, yaani mwezi mmoja na nusu hadi miwili baada ya kupanda, na pia
matunda yanatakiwa kuwa na urefu wa sentimita 15 mpaka 20, urefu pia unaweza
kutofautiana kulingana na aina ya matango yaliyopandwa. Baada ya mvuno wa
kwanza mkulima anaweza subiri wiki tatu kabla ya kuvuna mvuno wa pili.
Kiasi Cha
Mavuno
Ulimaji wa matango unaofuata
taratibu tajwa hapo juu hupelekea mavuno ya kiasi cha tani 6 mpaka 10 kwa ekari
moja na pia mtango mmoja unaweza zaa matunda matano hadi saba. Hii huweza
kutimia endapo mimea itatunzwa vizuri.
Hifadhi
Baada ya kuvuna matango yanatakiwa
kuhifadhiwa katika mazingira mazuri yenye kiwango cha unyevu wastani wa 90% hadi
95% na joto wastani nyuzi 10 hadi 13 za centigrade. Chini ya nyuzi joto 10
matango hubadilika rangi na kuwa ya njano hivyo kupunguza ubora wake. Matango
yasihifadhiwa kwa zaidi ya siku 14!
SOKO
Matango yana soko kubwa ndani na nje
ya nchi yetu. Biashara ya matango ndani ya nchi yanauzwa rejareja kwa bei ya
shilingi mia mbili hadi mia tano kwa tango moja. Hata hivo bei hutofautiana
kulingana na upatikanaji au uzalishaji wa matango wa mahali husika. Pia unaweza
kuuza kwenye migahawa, mahoteli na cafeteria.
Comments
Post a Comment