KILIMO NA NAMNA YA KULIMA MAINDI...Mahindi ni chakula muhimu na ni aina ya nafaka katika mataifa ya Afrika yaliyomo kusini mwa jangwa la Sahara

UTANGULIZI

Image result for KILIMO CHA MAHINDI
Mahindi ni chakula muhimu na ni aina ya nafaka katika mataifa ya Afrika yaliyomo kusini
mwa jangwa la Sahara. Ni chakula cha matumizi ya nyumbani kwa idadi ya watu
inayokadiriwa kuwa asilimia 50. Ni chanzo muhimu cha madini na kuongeza nguvu
mwilini, protini, madini ya chuma (iron) vitamini na madini mengine asilia.Waafrika
hutumia mahindi kwa njia mbalimbali (uji, ugali na pombe). Na mahindi ya kuchoma.
Kila sehemu ya mmea wa mahindi ina thamani kiuchumi : punje, majani, shina na magunzi
huweza kutoa kiasi kikubwa cha bidhaa nyinginezo zilizo chakula na zisizokuwa chakula.
Vile vile mahindi ni chakula muhimu cha mifugo (ng’ombe) na huhifadiwa kama silage. Pia
mabaki ya mimea na nafaka na pia hutumika viwandani kutengeneza wanga na mafuta.
Mahitaji ya mahindi katika hali ya hewa, udongo na Mahindi ni mimea ambayo hustahimili
mabadiliko mengi ya hali ya hewa na humea katika maeneo mengi tofauti. Kuna aina nyingi
za mahindi yanayotofautiana katika muda wa kukomaa, mahindi huwa na ustahimili
mkubwa kwa mabadiliko katika kiwango cha joto. Mahindi haswa huwa mimea ya maeneo
ya joto ambako unyevu ni wa kutosha.

HALI YA HEWA
Mmea huu unahitaji kiwango cha joto cha kila siku cha nyuzi joto 20º ili umee vyema. Joto
la juu sana kwa mazao mazuri ni kama nyuzi joto 30º. Hupandwa sana katika sehemu zilizo
katika kimo cha mita 3000 kutoka bahari hadi kwenye ukanda wa pwani. mahindi yaweza
kupandwa kama chakula cha mifugo. Hustawi vizuri katika udongo wenye uchachu wa
soil pH 6-6.5. Na pia Hustawi zaidi kwenye maeneo yenye mwinuko wa 2500m.
Mahindi huwa yanaathirika na ukosefu wa unyevu wakati wa kutoa maua na matunda. Pia
yanahitaji maji ya kutosha wakati wa kupanda. Katika nchi za joto jingi (tropiki), mahindi
hufanya vyema katika mvua ya kiwango cha milimita 600 hadi 900 wakati wa kukua.
Mahindi yanaweza kukuzwa kwenye aina nyingi za udongo lakini hukua vyema zaidi katika
mchanga, usiotuamisha maji mengi, ulio na hewa ya kutosha na ulio na rutuba na madini ya
kutosha. Kuwepo kwa mazao mengi ya mahindi kunapelekea kunyonywa sana kwa madini
kwenye udongo.
Mahindi yako katika kikundi cha mimea kinachoaminika kuathirika na hali ya chumvi
katika maji na udongo. Kwa vile mimea ambayo ni michanga huwacha sehemu kubwa bila
kuzingirwa na ardhi, mmomonyko wa udongo na kupoteza maji hutokea sana sana hivyo
basi ni bora umakini uzingatiwe katika uhifadhi wa udongo na maji kwa kuweka
matandazo (mulching).

KUTAYARISHA SHAMBA

 Tayarisha shamba la mahindi mara tu baada ya kuvuna mazao ya msimu uliopita.
 Mahindi hustawi sehemu yenye udongo wenye rutuba na usiosimamisha maji.
 Moto usitumike wakati wa kuandaa shamba.

FAIDA ZA KUANDAA SHAMBA MAPEMA

 Baada ya kuvuna,udongo bado ni mlaini hivyo hulimika kwa urahisi kwa kutumia
jembe lolote.
 Masalia yatakayofunikwa udongoni huoza mapema.
 Hupunguza magugu.
 Hupunguza wadudu waharibifu
 Mahindi yanapata mvua ya kutosha hadi kukomaa.
 Magonjwa kama yale ya ya majani (streak ugonjwa wa milia) hayatatokea au
yatakuwa kidogo.
 Mbolea uliyoweka itayeyuka pamoja na mahindi na yatastawi vizuri.

WAKATI WA KUPANDA

Wakati wa kupanda hutatanisha kwani mvua haitabiriki,Kama mvua hunyesha nyakati na
majira yale yale ya mwaka basi kalenda ifuatayo inaonyesha tahere za kupanda zao la
mahindi katika eneo lako.
 Mbeya na maeneo ya jirani, mwanzoni mwa mwezi Novemba hadi Desemba
mwishoni.
 Morogoro na maeneo ya jirani, Mwezi Januari katikati hadi Februari katikati
 Iringa na maeneo ya jirani, katikati ya mwezi Novemba hadi Desemba mwishoni
 Songea na maeneo ya jirani, katikati ya mwezi Novemba hadi Januari mwanzoni.
Kupanda mahindi mapema ni muhimu kwani uwezekano wa kuvuna mazao mengi ni
mkubwa. Kwa mashamba makubwa sana wakati wa kupanda uwe wiki moja kabla ya mvua
kuanza kunyesha na isizidi wiki mbili kabla ya mvua. Isiwe mapema zaidi kwani mbegu
zitaharibiwa na joto kati ya udongoni wadudu,panya,ndege na wanyama wengineo.

KUCHAGUA MBEGU BORA

Mbegu bora ni zile zilizo zalishwa kitaalamu.
 Ni safi hazijabunguliwa na wadudu.
 Huzaa mazao mengi.
 Hustahimili magonjwa.

AINA ZA MBEGU

 Mbegu aina ya chotara(hybrid)
 Aina ya ndugu moja(synthetic)
 Mbegu aina ya composite
Mbegu za kisasa zikitumiwa vizuri katika misingi ya kilimo zina uwezo wa kuzaa magunia
50-80 au tani 5.5 – 7.5 kwa hekta moja.

MAPENDEKEZO YA MBEGUZA KUPANDA

Kuna mbegu nyingi za kisasa zilizoko kwenye soko mfano wa SIDCO ,PANNAR, CHOTARA,
kutoka KENYA n.k


KUPANDA

Idadi ya mimea katika eneo ni muhimu kwani ikizidi
 Kuna uwezekano wa mazao hupungua.
 Mmea huangushwa na upepo
 Mabua mengi hayazai.
 Idadi ya mimea nayo ikipungua kwenya eneo husababishwa mavuno kupungua
jambo la kufanya ni kupanda mbegu katika nafasi sahihi zilizoshauriwa na mtaalamu
 hapo chini.
KIASI CHA KUPANDA
 Mbegu za mahindi huhifadhiwa kwa dawa kali(sumu)
 Kiasi cha kilo 20(ishirini) za mbegu kinatosha kupanda hekari moja., (*Hii hutegemea na aina ya mbegu)

NAFASI ZA KUPANDA.

Hiyo ni baina ya mstari na mstari na mche kwa mche.
 75cm x 30cm mfano:- mstari kwa mstari 75cm na mche kwa mche 30cm
 75cm x 60cm
 90cm x 25cm
 90cm x 50cm
PICHA: Nafasi nzuri ya upandaji

KUTUMIA MBOLEA

 Mahindi hustawi na kuzaa vizuri iwapo yatapatiwa mbolea pamoja na matunzo
mengine ya kilimo bora.
 Angalizo: Ukipanda mbegu bora bila kutumia mbolea ni kazi bure.

KUNA AINA MBILI KUU ZA MBOLEA

 Mbolea za asili mfano; samadi,mboji na majani mabichi,mbolea hizi hua na
virutubisho vya kutosha ambavyo havijulikani vipo kwa kipimo kiasi gani.
 Mbolea za viwandani, hizi hua na virutubisho vya kutosha na vipimo hujulikana, hii
inasaidia kujua ni kiasi gani kitumike kwa kipindi gani.
KWA MFANO:
Mbolea inayotumiwa na wakulima wadogo mara yingi huwa haitoshi. Mahindi ya kiwango
cha juu yaweza tu kufikia kiwango cha juu cha Uzalishaji iwapo yatapewa lishe na madini
ya kutosha. Mahindi ya tani 2 kwa hekta na tani 5 kwa hekta hutumia karibu kilo 60 N, kilo
10 za P205 na kilo 70 K20 kutoka katika udongo. MAhindi hunyonya Nitrogen pole pole
katika miezi ya kwanza baada ya kupanda, lakini huongezeka hadi kiwango cha juu kabisa
wakati wa kutoa maua na kukuza tunda (gunzi). Mahindi huhitaji nitrogen kwa kiwango
cha juu na ukosefu huwa ndio kizingiti. Kiwango cha juu cha nitrogen kinahitajika mara
tatu; kwanza wakati wa kupanda, pili, wakati ambapo mmea umefikia sentimita 50 za urefu
na tatu, wakati matunda ya mahindi yanaanza kutoa zile nyuzi nyuzi nyororo (silking).
Udongo mwingi huwa na madini ya phosphorous (P205) na potassium (K20) lakini sio
kiwango kinachotosheleza mahitaji haswa ya mbegu za mahindi zinapochipua. Nyunyuzia
P205 karibu na mbegu ili ziote kwa haraka. K20 hutumika kwa kiwango kikubwa lakini
hitaji la mimea hubainika baada ya upimaji wa hali ya udongo kujua kiasi cha mahitaji (soil
test). (ndo maana twasisitiza mbolea za viwandani sio lazima iwe ya chemical)

DALILI ZA UPUNGUFU WA MBOLEA

Ukosefu wa K20 husababisha ncha za majani kuwa na rangi ya njano na kuunda gunzi (cob)
lisilo na punje hadi juu. Ukosefu wa P205 hufanya matawi kuwa na rangi ya samawati na
mbegu zisizo laini. Dalili za ukosefu wa nitrogen ni majani ya rangi ya manjano na mimea
dhaifu mifupi. Phosphate haifyonzwi haraka na mahindi na pia udongo mwingi wa nchi za
joto hukosa madini hayo ya phosphate. Inashauriwa unyunyuzie mbolea ya kiasili kama
samadi kabla ya kulima ili uboreshe hali ya udongo na kuongezea madini.
Katika ukulima wa kiasili, (organic farming), Nitrogen (N) hutiwa kwenye udongo kupitia
kwa upandaji wa mimea ya jamii ya mikunde (legumes) ambayo hutoa nitrogen katika
hewa, Hata hivyo mapendekezo ya kimbolea yaliyo katika misingi ya uchunguzi wa udongo
hutoa nafasi nzuri ya kupata kiasi kizuri cha mbolea bila kuweka kiwango cha chini au juu.
Omba msaada kutoka kwa mafisa ugani wa kilimo waliyo katika eneo lako. Katika maeneo
yanayo tegemea mvua kukuza mahindi, panda mbegu wakati wa mvua ya kwanza. Hii
itaruhusu mizizi kunyonya madini yaliyotengenzwa na bakteria katika udongo. Maji
yaliyosimama huyeyusha na kuondoa madini ya nitrogen kutoka katika udongo na
kusababisha ukosefu wa Nitrogen.

KUDHIBITI MAGUGU

Udhibiti wa magugu ni muhimu sana. Katika wiki 4 hadi 6 za mbele baada ya kumea,
mahindi huathiriwa sana na magugu. Ni lazima mahindi yapandwe mara moja baada ya
kutayarisha shamba. Unaweza kulima katikati ya laini za mahindi ili udhibiti magugu.
Nchini Tanzania, kupalilia mara mbili kunahitajika kwa aina nyingi za mahindi, ingawa
kupalilia kwa mara ya tatu kutahitajika kwa aina ambazo zinahitaji miezi 6 hadi 8
kukomaa. Kupalilia kwa mikono kunahitaji siku 15 kwa hekta la mikono (power tiller) ni
masaa mawili mpaka matatu kwa ekari.

UHUSIANO WA NIPE NIKUPE

Desmodium (desmodium uncinatum) nyasi ya Molasses (melinis minutifolia) zikipandwa
kati kati ya laini za mahindi huzuia wadudu kama stalk borers moths. Mimea hii hutoa
kemikali ambazo huwafukuza wadudu aina stem borers’ moths. Zaidi ya hayo Desmodium
huzuia gugu haribifu,witchweed striga hermonthica. Napier grass (pennisetum
purpureum) na Sudan grass (sorghum vulgare sodanese) ni mimea mizuri sana
inayonasa wadudu aina ya stem borers.
Napier grass ina njia yake madhubuti ya kujikinga dhidi ya wadudu wanaotoboa mmea kwa
kutoa utomvu kutoka kwenye shina, ambayo huzuia wadudu kufyoza mmea na
kusababisha uharibifu. Nyasi hizi pia huvutia adui wa stem borers kama mchwa, earwigs na
buibui. Nyasi aina ya Sudan pia husaidia maadui asilia, kama nyigu (parasitic wasp).
Mahindi huweka kivuli kwenye mimea ya mboga mboga ikipandwa safu moja katikati ya
mboga kwenye maeneo yaliyo na jua kali. Hii huongeza mazao ya mboga zilizopandwa hivi.
na mimea jamii ya mikunde huongeza nitrogen kwenye udongo ambayo huitajika zaidi
katika ukuaji wa mahindi pia hupunguza wadudu aina ya (leafhoppers, leafbeatles, stalk
borers na fall army worm), upandaji wa mimea jamii ya mikunde ufanyike mara baada ya
palizi ya kwanza

UVUNAJI

Uvunaji hufanyika kwa kutumia mikono kwa mashamba madogo na mashine (combine
harvester) hutumika kwa ajili ya mashamba makubwa, Zao la wastani la mahindi
ulimwenguni mnamo mwaka 2000 lilikuwa kilogramu 4255 kwa kila hekta. Zao la wastani
nchini Marekani ilikuwa kilo 8600 kila hekta, huku mataifa yaliyo chini ya jangwa la Sahara
la Afrika yakivuna kilo 1316 kwa kila hekta ya shamba.
Zao la wastani katika taifa la Tanzania kati ya mwaka 2001-2005 lilikuwa kati ya gunia
15-19 kwa hekta (sawa na kilo 1350-1750) Ukilima kwa kuzingatia ukulima wa kisasa na
kanuni zake kwa Tanzania utavuna kilo 5000 kwa hecta (ukanda wa pwani) na kilo 7500
kwa nyanda za juu kama Iringa, Mbeya, Ruvuma, Arusha n.k

WADUDU NA MAGONJWA YA MAHINDI

WADUDU

1. Vipekecha shina wa mahindi (Busseola fusca; Chilo and Sesamia species)
Vipekecha shina wa mahindi ni wadudu waharibifu wa mahindi, mtama na mazao mengine
katika nchi nyingi za Afrika. Viwavi wa nondo, huchimba na kuingia ndani ya shina la
mahindi, wakila tishu za ndani na kusababisha mmea kunyauka na hatimaye kufa.
Wadudu hao wanaweza kudhibitiwa kwa njia mbalimbali kama mbinu za kitamaduni, hasa,
kilimo cha mseto na mfumo wa ‘sukuma-vuta’ (‘pushpull’). Pia wanaweza kudhibitiwa na
dawa za kuua wadudu, unga wa mwarobaini, lakini katika hatua za mapema, kabla ya
mabuu kuchimba na kuingia ndani ya shina.

2. Osama (Prostephanus truncates)
Dumuzi ‘Osama’ ni mdudu hatari sana wa mahindi ya kuhifadhiwa kote barani Afrika.
Osama hula ndani ya nafaka na kuacha shimo na ganda tupu. Ghala safi ya kuhifadhia ni
muhimu ili kuweza kuzuia uharibifu wa osama. Kukoboa nafaka kutoka kwa gunzi kabla ya
kuhifadhi kunaweza kupunguza uharibifu.

Funza wa vitumba (Helicoverpa armigera)
Funza wa vitumba ni mdudu msumbufu wa mimea mingi muhimu ya chakula, mafuta na
fedha duniani kote, ikiwa ni pamoja na nafaka mfano Mahindi ikiwa ni mojawapo, mikunde,
matunda na mboga. Ushambulizi mkali wa viwavi wa nondo huyu kunaweza kusababisha
hasara kwa mavuno yote.
Kudhibiti kwa njia ya kemikali kunapaswa kufanywa kwa makini na wakati mwafaka kwa
kuwa viwavi hutoboa na kuingia ndani ya nafaka au matunda ya mmea, hivyo kuweza
kulindwa. Usugu kwa dawa, kama vile za pyrethroid, kumeripotiwa katika nchi nyingi.
Bakteria aina ya Bacillus thuringiensis (Bt) na madawa ya mwarobaini hutoa udhibiti wa
ufanisi dhidi ya viwavi na wakati huo huo kupunguza uharibifu wa maadui wa kiasili.
Udhibiti muhimu wa kitamaduni ni pamoja na kuondoa na kuharibu mabaki ya mimea
baada ya kuvuna, kulima udongo ili uwatoe nje pupae na kupanda kwa wakati mmoja.


MAGONJWA

1. Doa jani la kijivu la mahindi (Cercospora zeae-maydis & Cercospora zeina)
Doa jani la kijivu la mahindi umeibuka kama ugonjwa ulioweka kikwazo kwa mazao ya
mahindi nchini Marekani na kusini mwa Afrika katika miaka 25 iliyopita. Ingawa
ulidhaniwa kuwa aina moja ya kuvu, Cercospora zeae-maydis, ukaguzi wa chembechembe
umeonyesha kuwa kuvu lingine, C. zeina, hupatikana kwa wingi mashariki mwa Marekani
na kusini mwa Afrika. Mbegu za kuvu, zinazoishi katika mabaki ya mazao ya awali,
hurushwa na matone ya mvua kwenye majani ya chini ya mmea na kusababisha madoa
marefu yanayoungana kwenye mimea isiyohimili na kusababisha baka. Mashina
hudhoofika na kuanguka wakati wa mikurupuko ya magonjwa.
Ugonjwa unaweza kusimamiwa kwa kuharibu mabaki ya mimea baada ya kuvuna, kilimo
cha mzunguko, kwa kutumia aina zinazovumilia ugonjwa zaidi, na, matumizi ya dawa za
kuua kuvu ikiwa zitaleta faida kiuchumi.

2. Muozo wa mahindi na mycotoxin (Fusarium and Aspergillus species)
Kuna aina nyingi za kuvu zinazotokea kwenye mahindi na kuzalisha sumu za kikemikali
ambazo huchafua chakula na lishe. Zinajulikana kwa pamoja kama mycotoxins, na sumu
hizi zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu na wanyama.
Aspergillus inasemekana kuwa mzalishaji muhimu zaidi wa mycotoxin katika Afrika,
ingawa kuvu nyingine kama vile Fusarium pia inahusika. Makundi yote mawili ya kuvu
hukua kwenye sehemu za mimea zilizokufa na zinazooza na kusababisha kuoza kwa
mahindi katika shamba. Huzalisha unga mwingi wenye mbegu za kuvu juu ya mahindi,
kabla na baada ya kuvuna, lakini pia inaweza kuwa bila kuzalisha koga lolote. Muozo wa
mahindi unaosababishwa na kuvu zinazozalisha mycotoxin hutokea kwa wingi zaidi wakati
mahindi yana matatizo na yanakua vibaya.
Udhibiti bora zaidi wa kuvu hizi huchanganya kuvuna kwa wakati muafaka na kukausha
mahindi kabla ya kuyahifadhi. Aflasafe™, njia mpya ya kibiolojia ya kudhibiti Aspergillus,
inatumika katika mashamba kabla ya mahindi kutoa maua na imeonyesha matumaini
makubwa katika kupunguza uchafuzi wa mahindi kabla ya kuvuna na baadaye mkusanyiko
wa mycotoxins katika bidhaa zilizohifadhiwa.

3. Ugonjwa wa maize lethal necrosis (Multiple virus infections)
Maize lethal necrosis disease (MLND) ni ugonjwa mpya wa virusi barani Afrika.
Umesababisha wasiwasi mkubwa kwa sababu mimea hufa na hakuna nafaka au ni nafaka
kidogo tu zinazozaliwa.
Chanzo cha ugonjwa
Wataalamu katika tafiti zao wanasema kuwa, ugonjwa huu husababishwa na virusi vya aina
mbili vinavyoathiri mmea wa mahindi kwa pamoja ambavyo ni Maize Chlorotic Mottle
Virus (MCMV) na Sugarcane Mosaic Virus (SCMV).
Virusi hivi husambazwa na wadudu wa aina mbili, ambao ni Thrips pamoja na Aphids, japo
kuna wadudu wengine wanaweza kubeba na kusambaza ugonjwa huo kama vile beetles
and leafhoppers pamoja na matumizi ya mbegu zilizoathirika.
 Dalili za mahindi yalioathirika
 Majani machanga ya juu hugeuka na kuwa na rangi ya njano na hatimaye kukauka
kuanzia pembezoni mwa jani kuelekea katikati na hatimaye mmea kufa.
 Mmea huweza kutoa machipukizi mengi sana.
 Mbelewele hukosa chamvua hivyo mmea kutozaa.
 Mahindi yakishambuliwa wakati yanajaza mbegu, gunzi husinyaa na kuweka mbegu
chache au kutojaza kabisa.
 Mahindi yaliyoathirika hushambuliwa na magonjwa nyemelezi hasa ukungu.
 Kwa mimea iliyoanza kusinyaa, huonyesha dalili za kukomaa kabla ya wakati, huku
hindi likiwa katika hali ya kuchoma maganda na kuonesha utayari wa kuvunwa.
Aidha, ugonjwa huo unaposhambulia katika hindi lililokomaa, basi huingia moja
kwa moja katika kiini cha punje.
Mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa huu huota fangas ambayo wataalamu wanasema
ina sumu kali ijulikanayo kama Aflatoxin. Sumu hiyo, husababisha madhara kwa
binadamu na wanyama.

Utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali wakiwepo wataalamu kutoka Taasisi ya utafiti
wa Kilimo ya Seliani (SARI) wamebaini kuwa, sumu hiyo (Aflatoxin) inayotokana na
fangasi, husababisha ugonjwa wa saratani ya ini kwa binadamu na wanyama. Utafiti huo
pia unaeleza kuwa, ugonjwa huo unaweza usionekane kwa haraka na huweza hata
kuchukua muda wa mwaka ndipo kujitokeza.
Hivyo basi, ni lazima mataifa yote kuwa makini na kuchukulia jambo hili kwa uzito zaidi.
Mbinu za kuepuka ugonjwa huu
• Panda mbegu bora zilizothibitishwa na Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI)
nchini.
• Usipande mbegu zilizovunwa msimu uliopita kutoka katika shamba lililoshambuliwa na
ugonjwa.
• Safisha shamba kwa kuondoa magugu na masalia yote ya mazao na
kuyachoma/kuyafukia kuepuka maficho ya wadudu na virusi vya ugonjwa. Kagua shamba
mara kwa mara na kama utaona dalili zilizotajwa hapo juu, toa taarifa kwa mtaalamu wa
kilimo aliye karibu nawe.
Namna ya kudhibiti
• Ng’oa mapema mahindi yote yaliyoathirika, na kuyateketeza haraka.
• Usipande mahindi katika shamba lililoathirika angalau kwa msimu mmoja. Panda mazao
mengine kama vile viazi mviringo, mihogo kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa
kilimo.
• Katika maeneo yenye ugonjwa, dhibiti wadudu wasambazao ugonjwa huo kwa
kunyunyizia kiuatilifu kulingana na maelekezo ya mtaalamu.
• Zingatia kilimo cha mzunguko wa mazao na toa taarifa mapema kwa afisa ugani wa kilimo
endapo utaona dalili za ugonjwa.
Ugonjwa wa MLND bado unafanyiwa utafiti kwa undani zaidi na dawa bado haijapatikana.
Hivyo wakulima wote wanatakiwa pindi wanapoona kuna dalili zozote zimeanza kujitokeza
katika mashamba yao, hawana budi kung’oa mimea yote bila kujali kama mengine
hayajaambukizwa kasha waziteketeze kwa moto. Hii ni kutokana na sababu kuwa hata
mimea ambayo bado haijaonesha dalili za kuambukizwa, hana budi kuonesha dalili
mapema kwani maambukizi husambaa kwa kasi sana na kwa muda mfupi.

4. Ugonjwa wa matupa kwenye mahindi (SMUT).
Ugonjwa huu hushambulia sehemu za uzazi za mahindi. Mashambulizi hufanywa na aina
mbili za vimelea jamii ya uyoga (ukungu) vijulikanavyo kwa majina ya kitaalamu
kama Sphacelotheca reliana na Ustilago maydis. Vimelea hivyo husababisha magonjwa ya
aina mbili ambayo dalili zake zinafanana. Mimea iliyoshambuliwa na ugonjwa huu ama
haizai kabisa ama inazaa kiasi kidogo ukilinganisha na jinsi ambavyo ingeweza kuzaa kama
isingekuwa imeshambuliwa. Kwa hiyo mashambulizi ya magonjwa haya husababisha
hasara ya mavuno.
Inakadiriwa kwamba hasara ya mavuno inawezakuwa kidogo tu ama asilimia kumi (10%)
au hata zaidi ya kiwango hicho, lakini kupoteza ni kupoteza hata kama ni kiwango kidogo.
Ugonjwa wa "matupa" unaosababishwa na kimelea kijulikanacho kama Ustilago
maydis hufahamika kama "Common Smut" kwa kiingereza.
Dalili zake huwa kuota kwa uvimbe katika sehemu za mmea zinazokua kama vile punje za
mahindi, mbelewele na hata kwenye majani. Uvimbe huo ukikauka na kupasuka hutoa
vumbi jeusi kama masizi ambayo ndiyo viini vya/mbegu ya huo ugonjwa. Dalili ya msingi
ya ugonjwa huu kwenye mhindi ni kwamba inawezekana kuwa na baadhi ya punje
zilizoshambuliwa na zingine ambazo hazina dalili katika gunzi moja.
Ugonjwa wa "smut" unaosababishwa na kimelea kijulikanacho kwa jina Sphacelotheca
reliana hufahamika kama "Head smut" kwa kiingereza. Kama ilivyo kwa ugonjwa wa
"smut" ya kawaida, dalili za ugonjwa huu hujitokeza mara nyingi katika hindi lenyewe na
mbelewele na mara chache katika shina la mhindi. Tofauti na ugonjwa wa "smut" ya
kawaida, katika ugonjwa huu badala ya mhindi kuathiriwa baadhi ya punje, hindi zima
hujaa vumbi jeusi ndani ambapo kwa nje ni kama mfuko mweupe ambao kabla ya kukauka
hufana na uyoga. Vumbi hilo jeusi ndilo viini vya kimelea. Vivyo hivyo kwenye mbelewele.
Wakati mwingine mmea ulioshambuliwa na ugonjwa huu hudumaa na hushindwa kuzaa.
Dalili nyingine ya ugonjwa huu ni mhindi kuotesha vijani vidogo badala ya mbelewele.
UDHIBITI WA MAGONJWA YA"SMUT"
1. Tumia mbegu bora ingawa mpaka sasa haipo mbegu maalumu yenye kustahimili
ugonjwa huu. Kwa kutumia mbegu bora, mkulima utajihakikishia mavuno bora.
2. Daima hakikisha unalima kilimo cha kisasa kikijumuisha urutubishaji wa udongo.
Epuka kuijeruhi mimea uwapo shambani. Mimea iliyo na majeraha hushambuliwa kwa
urahisi na ugonjwa huu. Pia dhibiti wadudu waharibifu ambao pamoja na
madhara mengine wanayosababisha pia huijeruhi mimea na kwa hivyo kurahisisha
maambukizo ya ugonjwa huu wa "smut".
3. Kila inapowezekana tumia kilimo cha kubadilisha mazao. Katika kubadilisha mazao ni
vema kutumia mzunguko wa mazao yasiyoshambuliwa na ugonjwa wa "smut" kama vile
ngano, shayiri, njegere, viazi na maharagwe.
4. Unapolima hakikisha masalia mabua yamefukiwa chini sana.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze kuhusu mbilimbili na matumizi yake yote

JUA KUHUSU UGONJWA WA BAWASIRI

jifunze kujua viazi mvirongo na faida zake hapa