Utangulizi
Baada ya bayogesi kuzalishwa, masalia ya samadi ambayo huwa imemeng’enywa hutolewa nje ya tanki la kuchachushia mara samadi mpya inapowekwa katika tanki, kupitia chemba maalum ya kuingizia mchamganyiko wa samadi. Samadi iliyomeng’enywa hutumika kama mbolea ya kukuzia mimea. Inafaa sana kwa kustawisha mimea ya aina mbalimbali.
Bayogesi (biogas) ni kitu gani?
Bayogesi
ni mchanganyiko wa gesi inayoundwa na viasilia mbalimbali
vinavyotengenezwa katika mazingira ya kutokuwepo hewa (oksijeni) ambayo
asilimia kubwa ni gesi ya methane (CH4). Bayogesi ambayo
aghalabu hutokana na kinyesi cha wanyama, masalia ya mimea na kinyesi
cha binadamu inaweza kuzalishwa na kutumika kupikia na hata matumizi
mengine kama vile kuendeshea mitambo mbalimbali. Matumizi ya gesi hii
kwa mtu ambaye ana mifugo kama vile nguruwe, ng’ombe yanaweza kusaidia
kuondokana na gharama za kununua nishati ya kuni, mkaa, umeme na hata
gesi asilia inayochimbwa ardhini. Gesi hii inapunguza gharama za
watumiaji wa vyanzo vingine vya nishati. Mfano, gharama za nishati ya
umeme na gesi asilia ni ghali sana hasa kwa mtumiaji atakayedhamiria
kutumia jiko la umeme au jiko la gesi lakini kwa
gesi hii ya samadi mtumiaji itamgharimu muda wake tu kujaza samadi na
maji kila siku na atakuwa hana malipo ya pesa kila mwezi kama
itakavyomlazimu kulipia umeme na gesi asilia kila mwezi, na hata kuni
ambazo watumiaji wengine hununua.
Mnyambulisho wa viambata Vya bayogesi
Kimsingi,
bayogesi huwa na mchanganyiko wa gesi za aina mbalimbali, lakini
inayopatikana kwa kiwango kikubwa ni gesi ya methane. Mgawanyiko huo kwa
asilimia ni kama ifuatavyo:-
Methane (50%)
Carbondioxide (25%)
Naitrojeni (10%)
Sulphur dioxide ( 5%)
Haidrojeni (1%)
Gesi nyingine (9%)
Zingatia
kwamba asilimia zilizooneshwa katika mabano zinaweza kubadilika
kutokana na malighafi inayotumika kutengeneza bayogesi (samadi, majani,
masalia ya chakula n.k.) na hali ya unyevunyevu wa malighafi hizo.
Uzalishaji wa bayogesi
Samadi
ghafi inayotokana na kinyesi cha wanyama (kama vile kuku, nguruwe,
ng’ombe na punda) kinaundwa na viasili vya Kaboni, Haidrojeni, Oksijeni
Naitrojeni na Salfa. Viasili hivi hutengeneza sukari, mafuta na protini.
Kinyesi au samadi humeng’enywa na bakteria ambao
huvunjavunja kinyesi hicho kutoka katika hali ya protini, mafuta na
sukari na kutengeneza muunganiko wa viasili ulio rahisi zaidi.
Mmeng’enyo wa samadi (kinyesi) kwa kutokuwepo wa gesi ya oksijeni
hutengeneza hewa ya ukaa (carbóndioxide). Mmengenyo wa samadi bila ya
uwepo wa oksijeni huzalisha gesi ya methane (CH4) ambayo ndio inayowaka hasa. Gesi hii itokanayo na kinyesi huzalisha kilojuli 5,200 hadi 5,800 kwa meta moja ya ujazo.
Bayogesi
huweza pia kuzalishwa kutokana na masalia ya mimea, kama vile masalia
ya zao la mkonge, masalia ya kakao au masalia ya kahawa baada ya
kutolewa ganda na nje. Malighafi hizi zote huweza kuzalisha bayogesi
iwapo zitachachushwa katika mazingira yasiyo na hewa (anaerobic
condition).
Aina za Mitambo ya Kuzalishia Bayogesi
Kuna aina kadhaa za mitambo ya kuzalishia bayogesi, ambayo inapatikana Tanzania. Aina hizi ni kama ifuatavyo.
Fixed Dome Biogas Digester (CAMARTEC/Hydraulic/Chinese)
Mitambo
ya aina hii ilianza kutengenezwa nchini China kuanzia mwaka 1936 na
ikasamabaa India mnamo mwaka 1937. Aina hii ya mitambo ya bayogesi
hujengwa katika maumbo ya mviringo wa nusu duara, na huwa na sehemu kuu
tano. Sehemu ya kwanza huwa ni sehemu ya kuchanganyia samadi na maji,
sehemu ya pili ni ya kuchachushia, sehemu ya tatu huwa ya kuhifadhia
gesi, sehemu ya nne ni ya kuhifadhia samadi ambayo imeshatumika
kuzalisha gesi. Sehemu ya tano ni ile ya matumizi, yaani jiko au oveni,
au jenereta.
Aina
hii ya mitambo hujulikana sana kama CAMARTEC (kufuatia kusambazwa kwa
wingi na kituo hiki cha kuhawilisha teknolojia za kilimo kwa ajili ya
matumizi vijijini, kituo hiki kipo mkoani Arusha). Lakini pia, mpango wa
serikali wa Miradi ya Gesi ya Samadi Dodoma (MIGESADO) ulijenga kwa
wingi sana aina hii ya mitambo katika mkoa wa Dodoma. Shirika lingine
linalohusika na ujenzi wa mitambo ya aina hii ni Shirika la Maendeleo na
Uholanzi (SNV), lenye tawi lake mkoani Arusha. Nao wanajenga kwa wingi
sana mitambo ya aina hii. Chanzo cha malighafi kwa mitambo hii ni samadi ya wanyama na kinyesi cha wanadamu.
Floating Drum/Gobar Biogas Digester
Aina hii ya mitambo sio maarufu sana kwa hapa kwetu Tanzania. Mitambo hii hutengenezwa kwa kutumia matanki makubwa ya plastiki (ya kuanzia ukubwa wa lita 1000), yanayobebana. Tanki kubwa
huwa linatangulia chini na ndilo ambalo huwa na malighafi kwa ajili ya
kutengenezea gesi. Tanki dogo hubebwa na hili kubwa, na huwa jepesi kwa
sababu linakuwa linabeba gesi, kwa hiyo huwa linaelea juu ya hili kubwa.
Tanki hili dogo huwa na kitu kizito cha kulikandamiza kwa juu yake, ili
lisiweze kutumbishwa na upepo uvumao. Malighafi inayotumika kuzalishia gesi kwa mitambo ya aina hii ni masalia ya chakula yatokayo majumbani na mahotelini
< 3.Vacvina Biogas Digester
Asili
ya mtambo huu ni nchini Vietnam, na inapatikana nchini Tanzania. Aina
hii ya mitambo huwa na sehemu kuu nne ambazo ni tanki la kuchanganyia
samadi na maji, tanki la kuchachushia samadi na kuzalishia gesi, tanki
la kuhifadhia samadi iliyokwishatumia, mirija ya kusafirishia gesi
kwenda katika vihifadhio, vihifdahio vya gesi (karatasi za nailoni
ngumu) na sehemu ya kutumia gesi (jiko, oveni au jenereta). Matanki ya
mtambo huu hujengwa kwa matofali ya kuchoma na saruji au matofali ya
mchanga na saruji. Vitako vyaa matanki haya hujengwa kwa zege, ili
kuongeza uimara na kuhimili uzito wa mchanganyiko wa samadi na maji.
Picha
hiyo hapo juu inaonesha matanki ya kuchachushia masalia ya mkonge kwa
ajili ya kuzalishia bayogesi, katika kiwanda cha mkonge kilicho Hale
mkoani Tanga
4. Plastic Bag Biogas digester
Hii
ni aina nyingine ya mitambo ya bayogesi ambayo inapatikana Tanzania.
Uchachushaji wa malighafi kwa ajili ya kuzalisha gesi kwa kutumia mtambo
huu hufanyika kwenye mfuko mgumu sana wa plastiki, ambao huwa na sehemu
ya kuingizia mchanganyiko wa samadi na
maji, na sehemu ya kutolea gesi kwwenda kwenye matumizi. Mfuko huu
mgumu wa plastiki aghalabu hufukiwa ardhini ili kuulinda dhidi ya jua
kali na kutoboka kutokana na shughuli za kibinadamu. Kwa aina hii ya
mtambo, gesi huhifadhiwa katika sehemu ya juu ya mfuko huu, kabla
haijasafirishwa kwenda kwenye matumizi. Mtambo huu ni wa gharama rahisi
kidogo ukilinganisha na mingine ambayo imeorodheshwa hapo juu, kutokana
na kutohitaji ujenzi unaohusisha matofali, zege ama saruji. Lakini shida
yake ni kwamba mifuko hii haipatikani kwa urahisi hapa Tanzania, mara
nyingi huagizwa kutoka nje ya nchi.
Matumizi ya Bayogesi
Nishati katika Majiko
Bayogesi
kutumika kama nishati katika majiko, kuendeshea mitambo kama vile
magari na jenereta za kuzalishia umeme. Kwa Tanzania, bayogesi imekuwa
ikitumika katika majiko maalum ya gesi kwa kupikia aghalabu na watu
wenye mifugo ambao wana uhakika na upatikanaji wa samadi.
Picha: Majiko yanayotumia bayogesi
Nishati ya Kuendeshea Mitambo (mashine, magari, jenereta za kuzalishia umeme)
Bayogesi
hutumika kuzalisha umeme. Mfano mzuri ni mtambo wa kuzalisha umeme ulio
katika mashamba ya Katani Limited yaliyo katika mji wa Hale mkoani
Tanga. Mahali hapo kuna jenereta ya ukubwa wa kilowati 150 kwa ajili ya
kuzalisha umeme, ambayo huendeshwa kwa kutumia bayogesi. Kabla ya gesi
kutumika katika mitambo, kwanza huchujwa kwanza katika chujio maalum
lililo na kemikali za madini ya chuma, ili kuondoa gesi ya ‘hydrogen
sulphide’ (H2S) ambayo huathiri sana mitambo kwa kusababisha kutu. Hali
kadhalika, hewa ukaa (CO2) nayo huondolewa katika mfumo huu wa uchujaji
huu, ili kufanya gesi ya methane iwe safi kabla ya kutumika katika
mitambo husika. Kwa gesi inayotumika kuendeshea magari, yenyewe hupozwa
kabisa na kuwa katika mfumo wa kimiminika, ili iwe rahisi kuhifadhiwa na
kutumika. Magari ya namna hii yanapatikana nchini Sweden.
Picha:
Jenereta ya kuzalisha umeme, inayoendeshwa kwa kutumia bayogesi. Ina
ukubwa wa kilowati 150 na inapatika katika kiwanda cha mkonge cha Katani
Limited, kichopo Hale Mkoani Tanga. Aliyesimama hapo kwenye jenereta ni
Mhandisi Gilead Kissaka, meneja wa kiwanda .
Mbolea Itokanayo na Samadi Iliyokwishameng’enywa
Baada ya bayogesi kuzalishwa, masalia ya samadi ambayo huwa imemeng’enywa hutolewa nje ya tanki la kuchachushia mara samadi mpya inapowekwa katika tanki, kupitia chemba maalum ya kuingizia mchamganyiko wa samadi. Samadi iliyomeng’enywa hutumika kama mbolea ya kukuzia mimea. Inafaa sana kwa kustawisha mimea ya aina mbalimbali.
Nahitaji kutengenezewa mtambo wa biogas nipo Dar es salaam 0782603069
ReplyDelete