kilio cha vitunguu


Vitunguu ni moja ya zao la bustani linalopendwa na kutumiwa kwa wingi sana si hapa nchini tu bali duniani kote kwa ujumla. Linachukua nafasi ya pili baada ya nyanya. Kitunguu kinatumika katika kachumbari, kama kiungo kwenye kitoweo kama vile Samaki, nyama, mboga za mahani n.k. Majani ya vitunguu hutumika kama mboga. Vitnguu pia hutumika kuandalia supu.



Vitunguu hustawi maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na maeneo yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa kwa vitunguu.

Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha, unaoruhusu mizizi kupenya na unaohifadhi unyevu kama vile udongo wa nusu mfinyanzi nusu tifutifu.

UPANDAJI WA MBEGU ZA VITUNGUU KWENYE KITALU.

Hapa kwetu Tanzania upandaji huanza mwezi March hadi Mei kutegemea na msimu wa kilimo ulivyo. Hivyo kilimo hiki huanza mara baada ya mvua kubwa za masika kumalizika. Kipindi cha kiangazi na baridi huruhusu ukuaji mzuri wa vitunguu.

Mbegu za vitunguu huoteshwa mapema katika kitalu. Mbegu zinaweza kutawanywa au kupandwa kwa mistari katika tuta la kitalu.Tengeneza matuta yenye upana wa mita 1 na urefu wowote kutegemea na mahitaji yako.Weka mbolea ya samadi ndoo moja hadi mbili kwa mraba wa mita moja.
Lima tuta kiasi cha sentimita 10-25.
Sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 15 kutoka mstari hadi mstari Katika upandaji wa mstari mbegu hupandwa katika nafasi ya sm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari. Gramu 5 (kijiko cha chai) zinatosha kusia eneo la mraba mita moja.
Tandaza nyasi na mwagilia.


Baada ya kupanda mbegu hufunikwa na udongo mwepesi na baadaye matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli miche michanga. Mbegu za vitunguu huota baada ya siku 7 hadi 10.

KUMBUKA KAMA UNATAKA KUWA MKULIMA NA ULIME ZAO LA VITUNGUU: Kilo 1.5 za mbegu zinatosha hekari moja ya shamba.
KUPANDIKIZA MICHE BUSTANINI(kutoka kwenye kitalu kwenda shambani)

Upandikizaji wa miche ya vitunguu hufanyika baada ya miche kukua na kufikia unene wa Penseli. Mara nyingi miche hii hukaa kwenye kitalu kwa siku 40 baada ya kupandwa.

Usichelewe kuhamishia miche yako bustanini maana ukipandikiza miche mikubwa itaanza kutoa maua badala ya kitunguu (bulbs). Hivyo mara nyingi miche ya namna hii hubaki na suke la maua.

Wakati wa kupandikiza usikate wala kupunguza majani. Miche ipandikizwe sm 30 kati ya mstari na mstari na sm 10 kati ya mche na mche.

Upandaji katika bustani hufanyika kwenye mistari katika matuta au kwenye vijaruba. Vijaruba hutumika katika maeneo tambarare na yenye ukame ili kuhifadhi unyevu baada ya kumwagilia. Sehemu zenye udongo mzito na wenye maji mengi tumia matuta yenye mwinuko wa sm 10 hadi sm 15 kutoka usawa wa ardhi.
KUMBUKA: Pandikiza miche wakati wa asubuhi au jioni na mwagilia maji ya kutosha lakini hakikisha maji hayatuami.

UWEKAJI WA MBOLEA

Weka mbolea ya kukuzia katika wiki ya nne hadi sita baada ya kupandikiza. Weka mbolea kwenye mstari na hakikisha isigusane na mimea. Hakikisha udongo una unyevu wa kutosha wakati wa kuweka mbolea. Tumia UREA au SA.

UMWAGILIAJI


Zao la vitunguu linahitaji maji katika kipindi chote cha ukuaji wa mmea na hasa wakati wa utungaji wa tunguu (bulb).

Katika kipindi kisicho na mvua, miezi ya mei hadi Agost, umwagiliaji ufanyike mara moja kwa wiki Pia katika umwagiaji hutegemea sana na aina ya udongo katika shamba lako kwa sisi wataalamu kama tunajua aina ya udongo uliopo shambani kwako tutaweza kukuambia inatakiwa umwagilie kwa muda gani na unatakiwa umwagilie tena baada ya siku ngapi.


Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu, unashauriwa kupunguza kiasi cha maji kadri vitunguu vinapoendelea kukua. Pia ni vema uache kumwagilia maji wiki nne hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa vitunguu na kuvuna ni siku 90 hadi 120 kutegemeana na aina ya mbegu.



KUDHIBITI MAGUGU(PALIZI) NA KUPANDISHIA UDONGO.

Kitunguu ni zao lisiloweza kuvumilia magugu, magugu husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha kudumaa kwa kitunguu.

Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kung'olewa kwa kutumia jembe dogo la mkono, kung'olea kwa mkono au kwa kutumia madawa ya kuulia magugu (herbicides).

KUMBUKA: Unapotifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu maana utaharibu udongo na vitunguu vyenyewe kwa kuwa mizizi ya vitunguu ipo juu juu sana.


Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kwamba mashina ya vitunguu vyako yako ndani walau sm 5. Pia kuna aina nyingine ya vitunguu ambavyo hutoa au hupandisha tunguu lake juu ya udongo vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu sana.
Hakikisha shamba linakuwa safi. Wakati wa kupalili, mkulima asichimbue sana udongo ili kuepuka mikwaruzano kwenye shina la vitunguu. Inulia udongo kwenye mashina kama mkulima amepanda sesa.

MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU.

Wadudu waharibifu.
Kuna aina mbili za wadudu wanaoharibu hili zao;

1. Viroboto wa vitunguu

Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao vitunguu hapa nchini kwetu Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wakati wa mavuno. Wadudu hawa huonekana hasa kipindi cha joto.

Dalili.

Majani yaliyoshambuliwa na wadudu hawa huwa na mabaka meupe yenye kung'aa. Katika hali iliyokithiri majani yote huwa na tabaka jeupe au kijivu na baadaye hunyauka kabisa.

Kuzuia.

Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa ya kuulia wadudu (insecticide) kama vile Marathion, Thiodan-35, Parathion

Ili kupunguza uvamizi mkubwa panga kupanda vitunguu mapema ili kipindi cha joto kinapofika kikute vitunguu vyako vimekomaa.

Epuka kupanda vitunguu katika shamba lililokuwa limepandwa jamii ya vitunguu hapo kabla kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k.
3. Bungua weupe (White grub)
Huyu ni aina ya funza mkubwa,. Hutaga mayai yake kwenye uozo wa majani na samadi na hivyo mashamba ya vitunguu yaliyoko karibu hata kwenye maeneo au mashamba karibu huwa kwenye hatari zaidi. Mdudu huyu huathiri kitunguu kwa kukata miche na minyoo wa vitunguu.
Hushambulia mizizi na kusababisha kukauka kwa mimea.
 Kutifulia shamba na kuwaweka wazi wadudu hawa kunapunguza idadi yao.
Pia Hawa huzuiwa kwa kuzingatia mzunguko wa mazao

MAGONJWA.

1. Ukungu mweupe.

Ugonjwa huu huonekana wakati wa baridi ulioambatana na unyevu mwingi angani.

Dalili.

* Utaona unga unga wa rangi ya zambarau katika majani.
* Majani hugeuka rangi na kuwa ya njano na kisha hunyauka.
* Ugonjwa huu hupenya hadi chini kwenye tunguu na husababisha kuoza.

KUZUIA

Fanya kilimo cha mzunguko ukihakikisha unapanda mazao mengine yasiyo jamii ya vitunguu. Panda vitunguu tena baada ya miaka mitatu kama athari ilikuwa kubwa.

Tumia dawa za ukungu (fungicides) kunyunyizia katika shamba. Hii ifanyike kabla ya dalili kuonekana. Tumia dawa kama Zineb ya unga, Maneb, Dithane M45, n.k.

Wakati unapoona dalili za hali ya hewa yenye baridi ikiambatana unyevunyevu angani. Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya siku sita ili kuzuia ugonjwa kuingia.
Ugonjwa ukishaingia kwenye mmea hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponesha.

2. Ukungu wa kahawia.

Ugonjwa huu huleta madhara makubwa wakati vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vitunguu viko ghalani.

Dalili.

Vikovu mbonyeo hujitokeza kwenye majani na baadaye huwa na rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na kutengeneza vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko katika jani zima au katika shina la kitunguu. Baada ya wiki kama tatu tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani yote huanguka na kidmsha kukauka.

Ugonjwa huu hushambulia kitunguu hata baada ya kuvuna kupitia sehemu ya shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu, kidonda au mkwaruzo.

 NAMNA YA KUZUIA

*Katika bustani, unapoona kitunguu kina dalili ya ugonjwa huu, ng'oa na choma.
* Kwa kinga ya bustani, piga dawa za Dithane M45 na dawa zingine za ukungu. Dawa hizi hupunguza uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa huu.
* Tumia kilimo cha mzunguko wa mazao katika eneo la bustani yako. Usipande vitunguu katika mzunguko wa jamii ya vitunguu.
* Wakati wa kuvuna epuka kukata vitunguu na kusababisha vidonda na makovu.
* Ukishavuna anika kwa siku mbili kabla ya kuhifadhi kwenye magunia.

3. Ugonjwa wa kuoza mizizi

Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na huenezwa na vimelea vya Ukungu (fungi).

Dalili

Mizizi kugeuka rangi na kuwa njano na kisha zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi hufa kwa kunyauka.

KUZUIA

Panda vitunguu kwa mzunguko wa mazao. Epuka kurudia kupanda vitunguu kwa mfululizo.

Panda aina za mbegu zinazostahilimili magonjwa kama;
Excel, L36, Granex, White Granex, Red creole.

4.  Ugonjwa wa doa la pinki (Purple blotch)

Uanza kama doa dogo linalozama ndani ya jani na kisha
linaongezeka ukubwa na kufanya rangi ya pinki. Kiini cha ugonjwa
huu huanzia kwenye mbegu na pia hubaki kwenye maozo ya majani
ya vitunguu. Aina ya Red Creole inaonyesha kutoshambuliwa sana
na ugonjwa huu.
Ugonjwa wa doa la pinki 
Kuoza kwa kitunguu
Mbinu za kudhibiti ugonjwa huu ni kuendesha mzunguko (crop
rotation) wa muda mrefu wa mazao pamoja na kuzuia kutuama kwa
maji shambani. Kupunguza msongamano wa mazao shambani na
matumizi ya mbolea zenye calcium, phosphate and potassium
hupunguza kuenea kwa ugonjwa huu. Kwa upande mwingine,
matumizi ya mbolea ya nitrojeni kwa wingi au kwa kiasi pungufu
uongeza mlipuko wa magonjwa. Viatilifu kama vile Mancozeb
hutumika kuzuia mashmbulizi ya ugonjwa huu.

UVUNAJI WA VITUNGUU


Kwa ujumla uvunaji wa vitunguu huanza siku 90 hadi 150 tangu kwa miche kupandwa yaani miezi mitatu hadi mitano tangu kupandikizwa bustanini kutegemeana na mbegu iliyopandwa.

Utagundua kuwa vitunguu vyako viko tayari kuvunwa unapoona karibu 50% au zaidi ya mazao shambani yanaanguka au majani kukauka.

Ili kurahisisha ukaushaji wa vitunguu, pangilia muda wako ili uvunaji ukutane na kipindi cha joto na kiangazi.
Uvunaji ufanywe kwa kung'oa baada ya kumwagilia maji bustani siku moja kabla ya kuvuna.
Baada ya kuvuna, kata majani sm 2 juu na kata mizizi sm 2 chini. Usikate chini sana ya shingo maana husababisha jeraha na kupelekea kitunguu kuoza.
KUMBUKA:Ucheleweshaji wa uvunaji unasababisha vitunguu kuoza na kuharibikia shambani. pia Tumia jembe la mkono na hakikisha vitunguu havikwaruzwi wakati wa kuvuna. Unaweza kuvuna tani 30-40 kwa hekta.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze kuhusu mbilimbili na matumizi yake yote

JUA KUHUSU UGONJWA WA BAWASIRI

jifunze kujua viazi mvirongo na faida zake hapa